SOMO KUTOKA KARIAKOO NA KIU YA FEDHA

Katika pitapita zangu, jana niliingia duka moja maeneo ya kariakoo, nikawakuta kina dada watatu ndani.

Mmoja akanipokea, wawili walikuwa bize na simu zao.

Lengo langu lilikuwa kununua simu. Nikauliza maswali mengi kwani nilihitaji kuelewa uwezo wa simu kabla sijanunua.

Bw. Brian Trancy Katika kitabu chake cha MARKETING aliandika,

Wanunuzi wengi ni waoga wakununua kwa sababu wanaogopa kupata hasara kwa kununua bidhaa isiyokidhi matarajio yao.

Usemi wa Bw. Trancy, ukawa kweli kwangu, kwani nilimdadisi dada kwa maswali mengi.

Mara nikaona uso wa dada unaanza kubadilika, akaboreka. Sauti yake ikaashiria aina flani ya ukali.

Wale kina dada wengine walikuwa bize na simu zao. Hawakunitazama kabisa.

Ndani ya moyo wangu, nilikuwa na kiu ya kupata elimu ya kina juu ya bidhaa ile ili nifanye maamuzi sahihi.

Pamoja na kugundua dada alikuwa ameboreka kwa maswali yangu, niliendelea kuporomosha maswali tu!

Mwisho, nikaamua kununua. Nilipotoa fedha, uso wa yule dada ukaanza kuonyesha tabasamu.

Wale kina dada waliokuwa wanachezea simu, wakaacha kwa muda.

Nao wakaja karibu wakitaka kuniuzia vitu vingine vinavyo pendezesha zaidi simu ile.

Wapo watu hadi waone fedha kwa macho ndio wanaonyesha umahiri feki. Hawajui fedha salama hujificha. Fedha inayokuja mbele mara nyingine ni chambo.

Tukio la kina dada hawa, likanifanya nitafakari zaidi kuhusu fedha.

Wengi wanapenda fedha lakini kwa tabia na maneno yao wanafukuza fedha!

Zipo tabia muhimu za kujifunza kuhusu fedha.

Fedha inahitaji heshima, haipendi itumike vibaya, haitaki dharau.

Fedha inapenda nidhamu. Nidhamu ya kujali wateja, na nidhamu ya kuandika matumizi.

Fedha haipendi mtu anayeboreka-boreka.

Fedha inapenda utulivu. Mtaalamu mwingine alisema, fedha haipendi kelele.

Ukienda bank yoyote kuna utulivu, hakuna kelele bank.

Ukienda Bank kuu, ndio kabisaa, kuna utulivu mkuu.

Ukiwa kwenye biashara au ofisini, mwisho wa siku unahitaji kipato kiongezeke, unahitaji fedha.

Mteja anapokuja ofisini au kwenye biashara yako, tambua kuwa anakusoma TABIA zako pia.

Jikite kwenye kutoa ELIMU ya kina kuhusu bidhaa au huduma yako.

Mteja yeyote anawasiwasi wa KUPIGWA (Yaani kupoteza fedha yake kwa kununua kitu kisichokidhi mahitaji yake).

Usikerwe na maswali ya wateja.

Hata kama wewe ni kiongozi, usipandishe pepo la hasira kutoka kwa wale unao waongoza.

Mtu akija ofisini kwako, onyesha ukarimu, onyesha unajali.

Ukarimu ulifanya watu zamani wapokee malaika bila kujua.

Pengine unaweza kuona jambo hili ni dogo, sio dogo, kwenye kutafuta fedha hakuna jambo dogo.

Ningekuwa nina mtazamo hasi, ningetoka dukani kwa dada yule na kwenda kununua duka lingine. Angepoteza mteja mmoja.

Mtaalamu mwingine alisema, mteja mmoja akipotea anapotea na wateja wengine kumi nyuma yake.

Sisemi wauzaji wote kariakoo wanafanya kama yule dada, la. Najua wapo wanao jua wajibu wao.

Kumbuka, Mteja au mtu akiuliza anataka kujua, usiboreke.

Jikite kwenye kutoa elimu ya kina kuhusu bidhaa au huduma yako. Fedha zipo.

Ili ufanye hivyo, IJUE vyema bidhaa yako. Ijue vyema ofisi yako. Fedha zipo.

Ukiwatumia wengine somo hili utasaidia kutoa elimu hii adhimu kwa maendeleo ya kila mmoja wetu.

Dr. Peter Mkufya
Kipunguni, Ilala Dar es Salaam.
www.petermkufya.com
+255 786 202 202

MKUFUNZI: https://chat.whatsapp.com/GJYDw4XzqLIF7LjBiIHJxb

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *